Polisi nchini Uchina wanamsaka mtu mmoja ambaye aliamua kumuuza mtoto wake wa kiume, baada ya kugombana na mke wake. 
Mtoto huyo aliuzwa kwa dola elfu tano. Kwa  mujibu wa BBC mke wa bwana huyo anayefanya katika mji mwingine alianza  kumkabili mume wake huyo ambaye ni mvivu na asiyependa kufanya kazi. Bwana huyo alimsubiri mkewe aende kazini na  kisha kumchukua mtoto wao na kumuuza kwa familia nyingine. Mama wa mtoto  huyo aligundua kuwa mwanaye ameuzwa aliporejea miezi kadhaa baadaye.
Mama huyo alimtafuta mwanae na kumpata, ingawa  familia iliyomnunua mtoto awali iligoma kumrejesha kwa madai kuwa  walikuwa wametia saini mkataba wa mauzo. Hatimaye familia hiyo ilikubali kumrejesha mtoto  huyo baada ya kurudishiwa dola zao elfu tano. Baba wa mtoto huyo  amekimbilia mafichoni.
Familia zilizohusika na sakata hilo zimegoma  kuzungumza na waandishi wa habari. Polisi pia wamekataa kusema lolote,  na mwandishi wa BBC aliambiwa na polisi hao-- Usitangaze kisa hiki,  kitatoa picha mbaya ya Uchina-- amenukuliwa polisi mmoja akisema.
PAKA NDANI YA FRIJI
Bwana mmoja nchini New Zealand amekutwa akiishi na paka wapatao sitini nyumbani kwani. Hata hivyo kwa sasa anakabiliwa mashataka ya  kutesa wanyama, baada ya paka wengine wapatao 38 kukutwa wamekufa na  kuhifadhiwa ndani ya friji lake.
Bwana huyo Donald Cruickshank mwenye umri wa  miaka 77, anadaiwa kuhifadhi mizoga paka hao kwa kuifunga na vipande vya  magazeti, na kuweka karibu na sehemu anayoweka chakula chake, ndani ya  friji.
Shirika la dhamana ya wanyama SPCA limesema  maafisa wake walikuta paka 19 wakirandaranda ndani ya nyumba ya bwana  huyo, wengine 17 walikuwa wamefungiwa, na paka wengine 23 wakiwa katika  ghorofa la chini katika hali mbaya ya kiafya.
Bwana huyo, ambaye amekana mashtaka yake  ameliambia gazeti la Herald kuwa aliwahifadhi paka hao ndani ya freezer  lake kwa takriban miaka mitatu, kwa sababu hakuwa na muda wa kuwazika.
