Ni zaidi ya miezi mitatu tangu Sudan Kusini  ilipojitenga na Sudan na kupata uhuru wake mwezi Julai mwaka huu. Kama  nchi mpya Sudan Kusini imekuwa ikianzisha taasisi mbali mbali za kitaifa  kama vile benki kuu, mahakama, bunge na fedha zitakazo tumiwa katika  nchi hii mpya. 
Lakini hata kwa kuzindua tasisi hizo, Sudan  Kusini bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo kutotambuliwa  kwa fedha zake na nchi jirani.
Ilhali ni jambo la kawaida kuweza  kubadilisha fedha za nchi yeyote katika benki mbali mbali haswa katika  nchi jirani, ni vigumu sana kubadilisha fedha za Sudan Kusini nchni  Uganda au Kenya na hasa nchini Ethiopia.
Katika Jimbo la Upper Nile linalopakana na  Jamhuri ya Sudan na Ethiopia, wafanyabiasha na wawekezaji kutoka  Ethiopia, waliohojiwa na BBC walilalamika kwamba kukataliwa kwa pauni za  Sudan Kusini na benki kuu nchini Ethiopia kunaathiri biashara zao.
"Tukiuza bidhaa zetu, ni lazima tutafute jinsi  ya kuenda Juba na kubadilisha hizi pauni na dola za Marekani ili tuweze  kwenda nyumbani na kununua bidha zingine au kuona familia zetu. Mara  nyingi kama msimu wa mvua, tunajikuta hatuwezi kuondoka kutoka Nasir kwa  sababu hakuna barabara kwenda Juba na inabidi tutegemee mashua ambazo  huchukua wiki mbili kufika au kumtuma mtu anayekwenda Juba akubadilishie  fedha. Kwa ajili hiyo, tunapoteza fedha nyingi sana" alisema Mulu Jelet  mchuuzi kutoka Ethiopia mjini Nasir, katika Jimbo la Upper nile.
Licha ya malalamiko ya wafayabiashara, meneja wa  benki moja mjini Gambella nchini Ethiopia ambaye hakutaka kutajwa jina  lake, alithibitisha kwamba hawachukui fedha za Sudan Kusini kwa sababu  hazikuwa na tarehe.
Nchini Kenya vile vile, fedha za Sudan Kusini  pia hazikubaliwi katika maduka ya kubadilisha fedha, jambo ambalo  linawatatiza wafanyabiashara na watu wanaojitafutia riziki katika nchi  hii mpya. Ofisi moja ya kubadilisha pesa iliyo mjini Nairobi ilisema  kwamba hawazichukui fedha za Sudan Kusini kwa sababu bado hawana uhakika  na thamani yake.
Licha na hili, raia wa Afrika mashariki walio  Sudan Kusini wanaendelea kuongezeka huku biashara kati ya nchi hizi  ukiendelea kukita mizizi kwani nchi hii mpya inaagiza zaidi ya asilimia  70 ya vyakula vyote na bidhaa za matumizi kutoka nchni jirani na hasa  Uganda na Kenya.

