| Mzee Michael Edward Kimemeta (picha na Dixon Busagaga) | 
Imeandikwa n Dixon Busagaga - Globu ya Jamii Moshi
Baba mzazi wa Muigizaji wa kike wa filami nchini maarufu kama Lulu,  ambaye anahusishwa na kifo cha marehemu Steven Charles Kanumba, ameibuka  na kueleza kushtushwa sana na taarifa za kifo hicho pamoja na habari  kuwa bintiye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na muigizaji huyo nguli  na kuwa anahusika na kifo chake.
 Baba Lulu, ambaye alijitambulisha kwa jina la Michael Edward  Kimemeta(49) mzaliwa wa Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro, kaiambia  Globu ya Jamii leo huko Moshi kuwa alimtambua Steven Kanumba kama  mwalimu wa mtoto wake Lulu,lakini hakuamini masikio yake baada ya kupata  taarifa za kifo hicho, huku bintiye, anayedaiwa alikuwa na mahusiano ya  kimapenzi na marehemu, anahusika.
Lulu alifikishwa mahakamani jana April 11, 2012 akikabiriwa na mashtaka  ya mauaji ya Marehemu Steven Kanumba, ikiwa ni siku nne baada ya kifo  cha msanii huyo. Alisema kuwa Elizabeth ama Lulu alizaliwa tarehe April  17,1995 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, na  kwamba alimaliza elimu ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya  Midway mwaka jana na kamba hivi sasa ana umri wa miaka 17. 
Bw Kimemeta alisema kuwa ni vyema polisi kuwa makini katika uchunguzi  wao kwa kuzingatia kuwa tukio hilo limejenga chuki na uhasama baina ya  Lulu na ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi wa marehemu Steven Kanumba.  Alisema kuwa kilichomshtusha zaidi ni taarifa za polisi kusema kuwa  kulitokea ugomvi kati ya Marehemu Steve Kanumba na Lulu,huku ikitajwa  kuwa walikuwa wapenzi.
“Hatukutegemea kama Marehemu Kanumba angeweza kuwa na mahusiano y  kimapenzi na binti yetu; kwanza ndiye tuliyekuwa tukimtegemea kwa kiasi  kikubwa katika kuendeleza na kukikuza kipaji alichokuwa nacho  Elizabeth”, alisema baba mtu. “Ninaomba Wanasheria na wanaharakati wa  haki za kibinadamu kuingilia suala hili na kusaidia katika kupatikana  kwa haki dhidi ya shtaka la mauaji linalomkabili binti yangu Elizabeth  na pia naomba swala hili lisichukuliwe kishabiki ama kwa hisia bali haki  ichukue mkondo wake”alisema.
![]()  | 
| Kanumba na Lulu mwaka jana. Picha kwa hisani ya Mpeli Jr Ngonywike | 
 Alisisitiza kuwa jamii inatakiwa kutambua mazingira ya  tukio hilo,ambapo chanzo kinasemekana ni ugomvi uliopelekea tafrani kwa  Lulu kutuhumiwa kumsukuma Marehemu Kanumba kwa kile kinachodaiwa kuwa  ulikuwa wivu wa kimapepenzi na haiyumkini hakukusidua kumuua hivyo yeye  anashangaa bintiye kuhusishwa moja kwa moja na mauaji. 
“Ushiriki wa mwanangu kuhusu mambo ya sanaa nilikwishapata wasiwasi na  mama yake mzazi alikuwa akiwasiliana na Marehemu Kanumba enzi za uihai  wake ambaye alikuwa anamhakikishia usalama wa Lulu na kusema kuwa  ataendele kubaki kama mwalimu…..lakini leo nasikia alikuwa ni mpenzi -  nilishtushwa” alisema Kimemeta. 
Baba Lulu pia ameelezea kusikitishwa kwake kwa kushindwa kuhudhuria  mazishi marehemu Steven Kanumba kuhofia usalama wake, na kusema  mazingira yatakaporuhusu hata sita kufika nyumbani kwa marehemu Steven  Kanumba na kutoa pole. Bw Kimemeta amesema kuwa anaungana na Watanzania  wote kutoa pole kwa familia ya Marehemu Steven Kanumba na kutoa mkono wa  pole kwa msiba huo mkubwa ambao haukutarajiwa.Kasema kuwa Kanumba  alikuwa bado ni kijana mdogo aliyeonyesha umahiri kwenye sanaa na kwamba  amecha pengo kwa familia yake na Tanzania kwa ujumla.

